Kuhusu
Tuzo kwa Mahakama inaahidi kutoa tuzo ya hadi dola milioni saba kwa taarifa kumhusu Talal Hamiyah, anayejulikana pia kama Ismat Mezarani. Hamiyah ndiye mkuu wa Shirika la Usalama wa Nje (ESO) la Hizballah, ambalo hudumisha vikundi vilivyopangwa kote ulimwenguni. ESO ndicho kitengo cha Hizballah kilicho na jukumu la kupanga, kuratibu, na kutekeleza mashambulio ya kigaidi nje ya Lebanoni. Mashambulio hayo kimsingi yamewalenga Waisraeli na Wamarekani.
Mnamo tarehe 13 mwezi Septemba, mwaka 2012, Wizara ya Fedha ya Marekani ilimtaja Hamiyah kama Gaidi wa Kimataifa Mwenye Sifa Maalumu kuambatana na Amri ya Rais 13224, kama ilivyorekebishwa, kwa kutoa msaada kwa shughuli za kigaidi za Hizballah Mashariki ya Kati na kwingineko ulimwenguni. Matokeo ya kutajwa huku, miongoni mwa matokeo mengine, ni kwamba mali yote na maslahi ya Hamiyah katika mali, vyote vilivyoko chini ya mamlaka ya Marekani vimezuiwa, na watu wa Marekani kwa jumla wamekatazwa kushiriki kwenye miamala yoyote na Hamiyah. Aidha, ni kosa la jinai kutoa kwa makusudi, au kujaribu au kula njama ya kutoa, msaada wa nyenzo au rasilimali kwa Hizballah, kundi lililotajwa na Marekani kama Shirika la Kigaidi la Kigeni.
