Kuhusu
Tuzo kwa Mahakama inaahidi kutoa tuzo ya hadi dola milioni tano kwa taarifa kumhusu Sajid Mir, anayejulikana pia kama Sajid Majid Chuhdri na Sajid Majid. Mir, kiongozi mwandamizi wa Shirika la Kigaidi la Kigeni (FTO) la Lashkar-e-Tayyiba (LeT) lililo na makao yake nchini Pakistani, anasakwa kwa kujihusisha kwake na mashambulio ya kigaidi ya mwezi Novemba, mwaka 2008 jijini Mumbai, India. Mir alikuwa meneja wa shughuli wa LeT kwa mashambulio hayo akitekeleza jukumu kuu katika kuyapanga, kuyaandaa, na kuyatekeleza.
Kuanzia tarehe 26, mwezi Novemba, mwaka 2008, na kuendelea hadi tarehe 29, mwezi Novemba, mwaka 2008, watu 10 waliopewa mafunzo na LeT walifanya msururu wa mashambulio yaliyoratibiwa dhidi ya shabaha mbalimbali mjini Mumbai, India, na kuwaua watu 166. Wamarekani sita walikuwa miongoni mwa waliouliwa wakati wa uvamizi huo ulioendelea kwa siku tatu: Ben Zion Chroman, Gavriel Holtzberg, Sandeep Jeswani, Alan Scherr, Naomi Scherr, na Aryeh Leibish Teitelbaum.
Mir amekuwa kiongozi mwandamizi wa LeT tangu takribani mwaka 2001. Kutoka mwaka 2006 hadi mwaka 2011, Mir alikuwa mkuu wa shughuli za nje za LeT na alipanga na kuelekeza mashambulio mbalimbali ya kigaidi kwa niaba ya kundi hilo. Hali kadhalika, Mir alidaiwa kula njama ya kutekeleza shambulio la kigaidi dhidi ya gazeti fulani na wafanyakazi wake nchini Denmaki kati ya mwaka 2008 na mwaka 2009.
Kwa jukumu lake katika mashambulio hayo ya Mumbai, Mir alifunguliwa rasmi mashtaka nchini Marekani mnamo mwezi Aprili, mwaka 2011. Mnamo tarehe 30 mwezi Agosti, mwaka 2012, Wizara ya Fedha ya Marekani ilimtaja Mir kama Gaidi wa Kimataifa Mwenye Sifa Maalumu kuambatana na Amri ya Rais 13224, kama ilivyorekebishwa. Matokeo ya kutajwa huku, miongoni mwa matokeo mengine, ni kwamba mali yote na maslahi ya Mir katika mali, vyote vilivyoko chini ya mamlaka ya Marekani vimezuiwa, na watu wa Marekani kwa jumla wamekatazwa kushiriki kwenye miamala yoyote na Mir. Aidha, ni kosa la jinai kutoa kwa makusudi, au kujaribu au kula njama ya kutoa, msaada wa nyenzo au rasilimali kwa FTO LeT. Mir yupo kwenye Orodha Magaidi Wanaosakwa Zaidi ya Shirika la FBI. Anaaminika kuishi nchini Pakistani.
