Kuhusu
Tuzo kwa Mahakama inaahidi kutoa tuzo ya hadi dola milioni kumi kwa taarifa kuhusu shughuli, mitandao, na washirika wa Muhammad Kawtharani, anayejulikana pia kama Jafar Kawtharani. Kawtharani ni kiongozi mwandamizi wa vikosi vya Hizballah nchini Iraki. Kawtharani alichukua baadhi ya majukumu ya uratibu wa kisiasa wa makundi ya wanamgambo, yaliyo nchini Iraki na yanayofungamana na Irani, ambayo awali yaliongozwa na marehemu jenerali Qasem Soleimani wa Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Kawtharani huwezesha shughuli za makundi yaliyo nje ya udhibiti wa Serikali ya Iraki ambayo yamezima maandamano kwa kutumia nguvu, yakashambulia balozi za kigeni, na kujihusisha katika shughuli pana za uhalifu uliopangwa. Kama mwanachama wa baraza la Kisiasa la Hizballah, Kawtharani amehimiza juhudi za Hizballah za kutoa mafunzo, ufadhili, na usaidizi wa kisiasa na ugavi na usafirishaji wa vifaa kwa makundi ya waasi wa dhehebu la Shia nchini Iraki. Kawtharani pia amesaidia wapiganaji wenye itikadi kali wanaoelekea Siria kuiunga mkono serikali ya Assad.
Mnamo tarehe 22 mwezi Agosti Mei, mwaka 2013, Wizara ya Fedha ya Marekani ilimtaja Kawtharani kama Gaidi wa Kimataifa Mwenye Sifa Maalumu kuambatana na Amri ya Rais 13224, kama ilivyorekebishwa. Matokeo ya kutajwa huku, miongoni mwa matokeo mengine, ni kwamba mali yote na maslahi ya Kawtharani katika mali, vyote vilivyoko chini ya mamlaka ya Marekani vimezuiwa, na watu wa Marekani kwa jumla wamekatazwa kushiriki kwenye miamala yoyote na Kawtharani. Aidha, ni kosa la jinai kutoa kwa makusudi, au kujaribu au kula njama ya kutoa, msaada wa nyenzo au rasilimali kwa Hizballah, kundi lililotajwa na Marekani kama Shirika la Kigaidi la Kigeni.
