Kuhusu
Tuzo kwa Mahakama inaahidi kutoa tuzo ya hadi dola milioni tano kwa taarifa kumhusu Mohammed Ali Hamadei, anayejulikana pia kama Ali Hamadei na Castro. Hamadei, anayedaiwa kuwa mwanachama wa Hizballah, anasakwa kwa jukumu lake katika utekaji nyara wa mwaka 1985 wa Ndege ya TWA 847.
Mnamo tarehe 14 mwezi Juni, mwaka 1985, magaidi waliiteka nyara ndege ya TWA Nambari 847 ikiwa safarini kutoka Athens kuelekea Roma. Kwa muda wa siku 17, ndege hiyo ililazimishwa kuvuka Bahari ya Mediterania ikiwa na abiria 153 na wahudumu, kutoka Beirut hadi Algiers na kurudi tena, ikatua Beirut mara tatu. Walipotua mara ya kwanza Beirut, watekaji hao walimchapa vibaya, kisha wakampiga risasi na kumuua mpiga-mbizi wa Jeshi la Majini la Marekani, Robert Stethem.
Mnamo tarehe 14 mwezi Novemba, mwaka 1985, Hamadei alifunguliwa rasmi mashtaka kwa jukumu lake na kushiriki katika utekaji nyara huo. Alikamatwa ndani ya Uwanja wa Ndege wa Franikfuti mnamo tarehe 12, mwezi Januari, mwaka 1987. Marekani ilitaka arejeshwe Marekani ili ashtakiwe, lakini Serikali Kuu ya Ujerumani ikaamua kumshtaki Ujerumani na, mnamo mwezi Mei, mwaka 1989, ikampata na hatia ya kuua, kushika mateka, kupiga watu, na utekaji nyara. Hamadei alihukumiwa kifungo cha maisha gerezani. Mnamo tarehe 15 mwezi Disemba, mwaka 2005, hata hivyo, aliachiliwa kutoka kizuizini. Hamadei alirejea Beirut, anakoaminika yuko.
Mnamo tarehe 12, mwezi Oktoba, mwaka 2001, Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Marekani ilimtaja Hamadei kama Gaidi wa Kimataifa Mwenye Sifa Maalumu kuambatana na Amri ya Rais 13224, kama ilivyorekebishwa. Matokeo ya kutajwa huku, miongoni mwa matokeo mengine, ni kwamba mali yote na maslahi ya Hamadei katika mali, vyote vilivyoko chini ya mamlaka ya Marekani vimezuiwa, na watu wa Marekani kwa jumla wamekatazwa kushiriki kwenye miamala yoyote na Hamadei. Aidha, ni kosa la jinai kutoa kwa makusudi, au kujaribu au kula njama ya kutoa, msaada wa nyenzo au rasilimali kwa Hizballah, kundi lililotajwa na Marekani kama Shirika la Kigaidi la Kigeni. Hamadei yupo kwenye Orodha ya Magaidi Wanaosakwa Zaidi ya Shirika la FBI.
