Kuhusu
Mkoa wa Khorasan wa Taifa la Kiislamu (ISIS-K) ni kundi la kigaidi lililo na makao yake nchini Afuganistanii na ambalo huendesha shughuli zake nchini Afuganistani na Pakistani. Likiwa limeundwa hasa na wanachama wa zamani wa Tehrik-e Taliban Pakistan, yaani Talibani wa Pakistani, na Vuguvugu la Kiislamu la Uzibekistani, ISIS-K liliahidi utii kwa ISIS mnamo mwaka 2015. ISIS-K ndio ilihusika na shambulio la bomu la mwezi Julai, mwaka 2016 kwenye maandamano ya amani mjini Kabul ambalo liliwaua karibu watu 80 na kuwajeruhi wengine 230. Mnamo mwezi Agosti mwaka 2016, kundi hili lilidai kuhusika na upigaji risasi na ulipuaji wa bomu la kujitoa mhanga kwenye hospitali moja Quetta, Pakistani, shambulio ambalo liliwaua watu 94. ISIS-K pia ilidai kuhusika na shambulio la mwezi Mei, mwaka 2020 kwenye hospitali ya uzazi ya Kabul ambalo liliwaua watu 24, wakiwamo watoto waliozaliwa karibuni, pamoja na mama zao.
Mnamo tarehe 14 mwezi Januari, mwaka 2016, Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Marekani ilitaja ISIS-K kuwa Kundi la Kigaidi la Kigeni chini ya kifungu 219 cha Sheria ya Uhamiaji na Uraia, kama ilivyorekebishwa. Hapo awali, mnamo tarehe 29 mwezi Septemba, mwaka 2015, Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje iliitaja ISIS-K kuwa Gaidi wa Kimataifa Mwenye Sifa Maalumu kuambatana na Amri ya Rais 13224, kama ilivyorekebishwa. Matokeo yake ni kwamba, mali yote na maslahi ya ISIS-K katika mali, vyote vilivyoko chini ya mamlaka ya Marekani vimezuiwa, na watu wa Marekani kwa jumla wamekatazwa kushiriki kwenye miamala yoyote na ISIS-K. Ni kosa la jinai kutoa kwa makusudi, au kujaribu au kula njama ya kutoa, msaada wa nyenzo au rasilimali kwa ISIS-K.
