Kuhusu
Tuzo kwa Mahakama inaahidi kutoa tuzo ya hadi dola milioni tano kwa taarifa kuhusu mauaji ya wafanyakazi wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) John Granville na Abdelrahman Abbas Rahama. Mnamo tarehe mosi, mwezi Januari, mwaka 2008, Granville na Rahama walikuwa wakielekea nyumbani baada ya karamu ya Mkesha wa Mwaka Mpya mjini Khartoum walipopigwa risasi na kuuliwa. Makundi mawili tofauti yalidai kuhusika na mauaji hayo: kundi ambalo sasa halipo tena la al-Qa’ida katika Ardhi ya Nile Mbili (AQTN) na Ansar al-Tawhid (Wafuasi wa Imani Kwamba Kuna Mungu Mmoja Tu).

Wanaume watano walishtakiwa na kupatikana na hatia kupitia mfumo wa sheria wa Sudani kwa kuhusika na mauaji hayo. Abdelraouf Abu Zaid Mohamed Hamza, Mohamed Makawi Ibrahim Mohamed, Abdelbasit Alhaj Alhassan Haj Hamad, na Mohanad Osman Yousif Mohamed walihukumiwa kifo kwa kunyongwa, lakini walitoroka kutoka gereza la Khober mjini Khartoum mwaka mmoja baada ya kupatikana na hatia. Mohanad anaripotiwa kufia Somalia mnamo mwezi Mei, mwaka in 2011. Abdelraouf alinaswa tena na mamlaka ya Sudani. Makawi na Abdelbasit wangali watoro. John Granville, umri wa miaka 33, aliyekuwa mfanyakazi wa shirika la kujitolea la Marekani la Peace Corps na mtafiti nchini Kameruni, alikuwa akifanyia kazi USAID kusini mwa Sudani kwa miaka zaidi ya mitatu. Kazi yake ilijikita katika programu za demokrasia na utawala, ambapo alisambaza redio zaidi ya 50,000 za majira zinazotumia nishati ya jua ili kuwasaidia wananchi wa eneo hilo kutumia haki zao na kujiandaa kwa ajili ya uchaguzi. Abdelrahman Abbas Rahama, umri wa miaka 39, alikuwa akifanya kazi na USAID tangu 2004 kama mmoja wa wanachama wa mwanzo wa Kikundi cha Kuitikia na Kusaidia Katika Janga la Darfur, Sudani cha USAID. Baadaye akawa dereva wa ujumbe wa USAID/Sudani mjini Khartoum.
