Kuhusu
Tuzo kwa Mahakama inaahidi kutoa tuzo ya hadi dola milioni tano kwa taarifa kumhusu Ali Atwa, anayejulikana pia kama Ammar Mansour Bouslim na Hassan Rostom Salim. Atwa, anayedaiwa kuwa mwanachama wa Hizballah, anasakwa kwa jukumu lake katika utekaji nyara wa ndege ya TWA Nambari 847 mnamo mwaka 1985.
Mnamo tarehe 14 mwezi Juni, mwaka 1985, magaidi waliiteka nyara ndege ya TWA Nambari 847 ikiwa safarini kutoka Athens kuelekea Roma. Kwa muda wa siku 17, ndege hiyo ililazimishwa kuvuka Bahari ya Mediterania ikiwa na abiria 153 na wahudumu, kutoka Beirut hadi Algiers na kurudi tena, ikatua Beirut mara tatu. Walipotua mara ya kwanza Beirut, watekaji hao walimchapa vibaya, kisha wakampiga risasi na kumuua mpiga-mbizi wa Jeshi la Majini la Marekani, Robert Stethem.
Mnamo tarehe 14, mwezi Novemba, mwaka 1985, Atwa alifunguliwa rasmi mashtaka kwa jukumu lake na kushiriki katika utekaji nyara huo. Mnamo tarehe 12, mwezi Oktoba, mwaka 2001, Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Marekani ilimtaja Atwa kuwa Gaidi wa Kimataifa Mwenye Sifa Maalumu kuambatana na Amri ya Rais 13224, kama ilivyorekebishwa. Matokeo ya kutajwa huku, miongoni mwa matokeo mengine, ni kwamba mali yote na maslahi ya Atwa katika mali, vyote vilivyoko chini ya mamlaka ya Marekani vimezuiwa, na watu wa Marekani kwa jumla wamekatazwa kushiriki kwenye miamala yoyote na Atwa. Aidha, ni kosa la jinai kutoa kwa makusudi, au kujaribu au kula njama ya kutoa, msaada wa nyenzo au rasilimali kwa Hizballah, kundi lililotajwa na Marekani kama Shirika la Kigaidi la Kigeni. Atwa yupo kwenye Orodha ya FBI ya Magaidi Wanaosakwa Zaidi. Anaaminika kuwa nchini Lebanoni.
