Kuhusu
Tuzo kwa Mahakama inaahidi kutoa tuzo ya hadi dola milioni saba kwa taarifa kumhusu Muhammad Abbatay, anayejulikana zaidi kama Abd al-Rahman al-Maghrebi. Al-Maghrebi ni kiongozi muhimu wa al-Qa’ida (AQ) aliye na makao yake nchini Iran. Ndiye mkurugenzi wa muda mrefu wa kitengo cha habari cha AQ, al-Sahab, na ni mkwe na mshauri mkuu wa kiongozi wa AQ Ayman al-Zawahiri.
Hati zilizopatikana wakati wa operesheni ya kijeshi mnamo mwaka 2011 dhidi ya kiongozi wa zamani wa AQ ambaye sasa ni marehemu Usama bin Ladin zinaashiria kwamba al-Maghrebi amekuwa nyota akipanda ngazi za uongozi wa AQ kwa miaka mingi. Al-Maghrebi ametumika kama meneja mkuu wa AQ nchini Afuganistani na Pakistani tangu mwaka 2012. Kufuatia shinikizo ya kimataifa kwa miaka mingi katika kukabiliana na ugaidi, alihamia Irani, ambako ameendelea kusimamia shughuli za AQ kote duniani. Kama mkuu wa Ofisi ya AQ ya Mawasiliano ya Nje, al-Maghrebi huratibu shughuli pamoja na washirika wa AQ.
Mnamo tarehe 12 mwezi Januari, mwaka 2021, Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Marekani ilimtaja al-Maghrebi kama Gaidi wa Kimataifa Mwenye Sifa Maalumu kuambatana na Amri ya Rais 13224, kama ilivyorekebishwa. Matokeo ya kutajwa huku, miongoni mwa matokeo mengine ni kwamba, mali yote na maslahi ya al-Maghrebi katika mali, vyote vilivyoko chini ya mamlaka ya Marekani vimezuiwa, na watu wa Marekani kwa jumla wamekatazwa kushiriki kwenye miamala yoyote na al-Maghrebi. Aidha, ni kosa la jinai kutoa kwa makusudi, au kujaribu au kula njama ya kutoa, msaada wa nyenzo au rasilimali kwa AQ, iliyotajwa na Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Marekani kuwa Shirika la Kigaidi la Kigeni.
