Shambulio la Bomu Dhidi ya Ndege ya Pan Am Flight 103

Mashariki ya Karibu - Afrika Kaskazini na Mashariki ya Kati | Ulaya na Eurasia

Tuzo

Hadi dola milioni 5

Fanya jukumu lako.

Kuhusu

Tuzo kwa Mahakama inaahidi kutoa tuzo ya hadi dola milioni tano kwa taarifa kuhusu shambulio la bomu dhidi ya Ndege ya Pan Am 103. Mnamo tarehe 21 mwezi Disemba, mwaka 1988, Ndege ya Pan Am 103, aina ya Boeing 747, ikiwa safarini kutoka Uwanja wa Ndege wa London Heathrow kuelekea Uwanja wa Ndege wa John F. Kennedy jijini New York, iliharibiwa ikiwa angani kwenye eneo la Lockerbie, Scotland wakati kilipukaji cha kujitengenezea, kilichokuwa kimefichwa kwenye mizigo, kilipolipuka. Mlipuko huo uliwaua abiria wote 259 na wafanyakazi waliokuwa ndani ya ndege hiyo, wakiwamo Wamarekani 190, na pia wakazi 11 wa eneo hilo waliokuwa ardhini. Shambulio hilo, lililopangwa na kutekelezwa na majasusi wa Libya, ndilo lililokuwa shambulio kubwa zaidi la kigaidi dhidi ya Wamarekani kabla ya tarehe 11 mwezi Septemba, mwaka 2001. Lingali shambulio baya zaidi la kigaidi katika historia ya Uingereza.

Mara tu baada ya mkasa huo, polisi wa Scotland na Marekani walifanya uchunguzi wa pamoja. Mnamo mwezi Novemba, mwaka 1991, mamlaka zilifungua mashtaka ya jinai kote Marekani na Scotland dhidi ya majasusi wa Libya Abdel Baset Ali al-Megrahi na Lamen Khalifa Fhimah.

Mnamo tarehe 31 mwezi Januari, mwaka 2001, al-Megrahi alipatikana na hatia kwa makosa yote, naye Fhimah akaachiliwa. Al-Megrahi alipata hukumu ya lazima ya kifungo cha maisha gerezani. Mnamo mwezi Agosti, mwaka 2009, aliachiliwa huru kutoka gerezani kwa misingi ya huruma baada ya kugunduliwa na saratani isiyopona. Al-Megrahi alifariki akiwa nyumbani kwake nchini Libya mnamo mwezi Mei, mwaka 2012.

Mnamo tarehe 21 mwezi Disemba, mwaka 2020, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Marekani ilitangaza mashtaka mapya dhidi ya jasusi wa Libya wa zamani, Abu Agela Mas’ud Kheir al-Marimi, kwa jukumu lake katika shambulio hilo.

Skip to content