Kuhusu
Tuzo kwa Mahakama inaahidi kutoa tuzo ya hadi dola milioni saba kwa taarifa kumhusu Salman Raouf Salman, anayejulikana pia kama Samuel Salman El Reda na Salman Remal. Salman huelekeza na huunga mkono shughuli za kigaidi za Hizballah maeneo ya Amerika Kaskazini na Kusini. Akiwa kiongozi katika Shirika la Usalama wa Nje (ESO) la Hizballah, Salman pia amehusika katika njama kote duniani. ESO ndicho kitengo cha Hizballah chenye jukumu la kupanga, kuratibu, na kutekeleza mashambulio ya kigaidi nje ya Lebanoni. Mashambulio hayo kimsingi yamewalenga Waisraeli na Wamarekani.
Salman anatathminiwa kuwa alitumika kama mratibu wa ardhini wa shambulio la bomu la mnamo tarehe 18 mwezi Julai, mwaka 1994 kwenye kituo cha jamii cha Shirika la Kusaidiana la Kiyahudi la Ajentina mjini Buenos Aires. Mlipuko wa kilipukaji cha kujitengenezea kilichotegwa ndani ya gari uliwaua watu 85 na kujeruhi zaidi ya 300.
Mnamo tarehe 19 mwezi Julai, mwaka 2019, Wizara ya Fedha ya Marekani ilimtaja Salman kama Gaidi wa Kimataifa Mwenye Sifa Maalumu kuambatana na Amri ya Rais 13224, kama ilivyorekebishwa. Matokeo ya kutajwa huku, miongoni mwa matokeo mengine, ni kwamba mali yote na maslahi ya Salman katika mali, vyote vilivyoko chini ya mamlaka ya Marekani vimezuiwa, na watu wa Marekani kwa jumla wamekatazwa kushiriki kwenye miamala yoyote na Salman. Aidha, ni kosa la jinai kutoa kwa makusudi, au kujaribu au kula njama ya kutoa, msaada wa nyenzo au rasilimali kwa Hizballah, kundi lililotajwa na Marekani kama Shirika la Kigaidi la Kigeni.
