Sayf al-Adl

Mashariki ya Karibu - Afrika Kaskazini na Mashariki ya Kati

Tuzo

Hadi dola milioni 10

Fanya jukumu lako.

Kuhusu

Tuzo kwa Mahakama inaahidi kutoa tuzo ya hadi dola milioni kumi kwa taarifa kumhusu Sayf al-Adl. Al-Adl aliye na makao yake nchini Irani ni kiongozi mwandamizi wa al-Qa’ida (AQ) na mwanachama wa baraza la viongozi wakuu la AQ, Majlis al-Shura. Al-Adl pia huongoza kamati ya kijeshi ya AQ.

Al-Adl alifunguliwa rasmi mashtaka na akashtakiwa na jopo kuu la kusikiliza kesi la mahakama ya serikali kuu ya Marekani mnamo mwezi Novemba, mwaka 1998 kwa jukumu lake katika mashambulio ya mabomu ya mnamo tarehe 7 mwezi Agosti, mwaka 1998 dhidi ya balozi za Marekani mjini Dar es Salaam, Tanzania, na Nairobi, Kenya. Mashambulio hayo yaliwaua raia 224 na kuwajeruhi wengine zaidi ya 5,000.

Baada ya mashambulio hayo ya bomu ya mwaka 1998 dhidi ya balozi za Marekani, al-Adl alihamia kusini-mashariki mwa Irani na akaishi chini ya ulinzi wa Kikosi cha Irani cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Mnamo Aprili, mwaka 2003, mamlaka za Irani zilimweka kwenye kizuizi cha nyumbani pamoja na viongozi wengine wa AQ.

Mnamo mwezi Septemba, mwaka 2015, al-Adl na viongozi waandamizi wengine wanne wa AQ waliachiliwa kutoka kizuizi cha Irani ili kuwabadilisha na mwanadiplomasia wa Irani aliyetekwa nyara na AQ nchini Yemeni.

Al-Adl alikuwa msaidizi mwandamizi wa Abu Musab al-Zarqawi, mwanzilishi wa AQ nchini Iraki, ambayo baadaye ilibadilika kuwa Dola la Kiislamu la Iraki na Siria (ISIS).

Mapema sana kama miaka ya tisini, al-Adl na majasusi wengine wa AQ walitoa mafunzo ya kijeshi na kijasusi kwenye mataifa mbalimbali, yakiwamo Afuganistani, Pakistani, na Sudani, kwa wanachama wa AQ na makundi shirika, likiwamo lile la Misri la Jihad ya Kiislamu.

Mnamo mwaka 1992 na mwaka 1993, aliwapa mafunzo ya kijeshi majasusi wa AQ na watu wa makabila ya Somali waliopigana dhidi ya majeshi ya Marekani mjini Mogadishu, wakati wa Operesheni Rejesha Matumaini.

Kama luteni kanali katika vikosi maalumu vya Misri mnamo katikati ya miaka ya themanini, alihusika na juhudi za kupindua serikali ya Misri. Mnamo mwaka 1987, alikamatwa pamoja na maelfu ya wapiganaji wengine walioipinga serikali baada ya jaribio la kumuua Waziri wa Mambo ya Ndani wa Misri. Mamlaka zilimwachilia huru kisha zikamshusha cheo al-Adl, ambaye mnamo mwaka 1989 alisafiri kwenda Afuganistani ambapo alikuwa mkufunzi wa kundi changa la AQ.

Mnamo tarehe 23, mwezi Septemba, mwaka 2001, al-Adl aliorodheshwa kwenye Kiambatanisho cha Amri ya Rais 13224, na kutokana na kuorodheshwa huku, amewekewa vikwazo chini ya amri hiyo kama Gaidi wa Kimataifa Mwenye Sifa Maalumu. Matokeo ya kutajwa huku, miongoni mwa matokeo mengine, ni kwamba mali yote na maslahi ya al-Adl katika mali, vyote vilivyoko chini ya mamlaka ya Marekani vimezuiwa, na watu wa Marekani kwa jumla wamekatazwa kushiriki kwenye miamala yoyote na al-Adl. Aidha, ni kosa la jinai kutoa kwa makusudi, au kujaribu au kula njama ya kutoa, msaada wa nyenzo au rasilimali kwa FTO AQ. Al-Adl yupo kwenye Orodha ya Magaidi Wanaosakwa Zaidi ya Shirika la FBI.

Skip to content