Kuhusu
Tuzo kwa Mahakama inaahidi kutoa tuzo ya hadi dola milioni kumi na tano kwa taarifa zitakazowezesha kuvurugwa kwa taratibu za kifedha za kikosi cha Irani cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) na matawi yake yote, kikiwamo kikosi cha IRGC-Kikosi cha Qods (IRGC-QF). IRGC imefadhili mashambulio na shughuli nyingi za kigaidi duniani. IRGC-QF huongoza shughuli za kigaidi za Irani nje ya Irani kupitia mawakala wake, kama vile Hamas, Hizballah, na makundi ya wanamgambo nchini Iraki yanayoungwa mkono na Irani.
Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Marekani inaahidi tuzo kwa taarifa kuhusu vyanzo vya mapato ya IRGC, IRGC-QF, matawi yake au taratibu muhimu za uwezeshaji wa kifedha, zikiwamo:
- mipango haramu ya kifedha ya IRGC, zikiwamo mafuta-kwa-pesa;
- Kampuni laghai zinazoonekana kama zinafanya biashara halali ambazo zinajihusisha na shughuli za kimataifa kwa niaba ya IRGC;
- Vyombo au watu binafsi wanaosaidia IRGC katika kukwepa vikwazo vya Marekani na vya kimataifa;
- taasisi rasmi za kifedha zinazofanya biashara na IRGC;
- Jinsi IRGC inavyohawilisha pesa na nyenzo hadi kwa magaidi na wanamgambo mawakala na wabia wake;
- Wafadhili wa IRGC au wawezeshaji wa kifedha;
- Taasisi za kifedha au nyumba za ubadilishanaji pesa zinazowezesha miamala ya IRGC;
- Biashara au uwekezaji unaomilikiwa au kudhibitiwa na IRGC au wafadhili wake;
- Kampuni laghai zinazoonekana kama zinafanya biashara halali zinazojihusisha na ununuzi wa kimataifa wa teknolojia inayoweza kutumika kwa malengo ya amani au ya kivity kwa niaba ya IRGC;na
- Mipango ya kihalifu inayohusisha wanachama na wafuasi wa IRGC, ambayo inalinufaisha kifedha shirika hilo.
Shirika la IRGC ambalo lilianzishwa mnamo mwaka 1979 baada ya Mapinduzi ya Irani ni tawi la majeshi la Irani. Kupitia Kikosi chake cha Qods, IRGC hutekeleza jukumu muhimu zaidi miongoni mwa wahusika wa Irani katika kuelekeza na kutekeleza kampeni ya kigaidi ya utawala huo kote duniani.
IRGC imehusika katika mipango ya kigaidi na inaunga mkono ugaidi kote ulimwenguni. IRGC imehusika na mashambulio kadha yaliyowalenga Wamarekani na majengo ya Marekani yakiwamo yale ambayo yamewaua raia wa Marekani. IRGC imeunga mkono mashambulio dhidi ya wanajeshi wa Marekani na washirika wake na ujumbe wa kidiplomasia nchini Afuganistani na Iraki.
Aidha, IRGC imewateka nyara na kuwazuia kimakosa watu wengi wa Marekani, wengi wao ambao bado wanazuiliwa nchini Irani leo.
IRGC–QF imepanga shughuli nyingi kubwa za kigaidi kote ulimwenguni, kwenye mataifa kama vile Bahareni, Bosnia, Bulgeria, Ujerumani, Kenya, Uturuki, na Marekani.
Mnamo tarehe 15 mwezi Aprili, mwaka 2019, Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Marekani ilitaja IRGC kuwa Shirika la Kigaidi la Kigeni chini ya kifungu 219 cha Sheria ya Uhamiaji na Uraia, kama ilivyorekebishwa. Mwaka 2017, Wizara ya Fedha ya Marekani ilitaja IRGC kuwa Gaidi wa Kimataifa Mwenye Sifa Maalumu kuambatana na Amri ya Rais 13224, kama ilivyorekebishwa, kwa shughuli zake za kuunga mkono IRGC-QF. Matokeo ya kutajwa huku, mali yote na maslahi ya IRGC katika mali, vyote vilivyoko chini ya mamlaka ya Marekani vimezuiwa, na watu wa Marekani kwa jumla wamekatazwa kushiriki kwenye miamala yoyote na IRGC. Ni kosa la jinai kutoa kwa makusudi, au kujaribu au kula njama ya kutoa, msaada wa nyenzo au rasilimali kwa IRGC.
