Kuhusu
Tuzo kwa Mahakama inaahidi kutoa tuzo ya hadi dola milioni tano kwa taarifa kumhusu Ibrahim al-Banna, anayejulikana pia kama Abu Ayman al-Masri. Al-Banna ni kiongozi mwandamizi wa al-Qa’ida Kwenye Rasi ya Kiarabu (AQAP), kundi lililotajwa na Marekani kama Shirika la Kigaidi la Kigeni (FTO). Alikuwa mwanachama mwanzilishi wa AQAP, ametumika kama mkuu wa usalama wa kundi hilo, na ametoa mwongozo wa kijeshi na kiusalama kwa uongozi wa AQAP. Al-Banna ndiye wa mwisho wa wanachama waanzilishi wa AQAP.
Kwenye makala ya mwaka 2010 kwa jarida la mtandaoni katika lugha ya Kiingereza la AQAP, Inspire, al-Banna alieleza mashambulio ya kigaidi ya tarehe 11 mwezi Septemba, mwaka 2001 dhdi ya Marekani kama yenye uadilifu na akatishia kuwalenga Wamarekani kote ulimwenguni kama jibu kwa vitendo vya Marekani ng’ambo. Kabla ya uanachama wake katika AQAP, al-Banna alikuwa kiongozi wa kundi la Jihad ya Kiislamu ya Misri nchini Yemeni kuanzia mwaka 1996 hadi mwaka 1998 na baadaye alikuwa mkuu wa vitengo vya kundi hilo vya mafunzo na ujasusi.
Mnamo tarehe 5 mwezi Juni, mwaka 2017, Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Marekani ilimtaja al-Banna kuwa Gaidi wa Kimataifa Mwenye Sifa Maalumu kuambatana na Amri ya Rais 13224, kama ilivyorekebishwa. Matokeo ya kutajwa huku, miongoni mwa matokeo mengine, ni kwamba mali yote na maslahi ya al-Banna katika mali, vyote vilivyoko chini ya mamlaka ya Marekani vimezuiwa, na watu wa Marekani kwa jumla wamekatazwa kushiriki kwenye miamala yoyote na al-Banna. Aidha, ni kosa la jinai kutoa kwa makusudi, au kujaribu au kula njama ya kutoa, msaada wa nyenzo au rasilimali kwa AQAP, kundi lililotajwa na Marekani kama Shirika la Kigaidi la Kigeni (FTO).
