Kuhusu
ISIS Afrika Magharibi (ISIS-WA), sehemu ndogo ya kundi la kigaidi la Boko Haram, ilibuniwa wakati ambapo ISIS-WA iliahidi utii kwa ISIS mnamo mwezi Machi, mwaka 2015. ISIS ilikubali ahadi ya kundi hilo, na likaanza kujiita ISIS-Afrika Magharibi. Kimsingi likiendesha shughuli zake kaskazini mashariki mwa Nigeria na kanda kubwa ya Ziwa Chadi, ISIS-WA limetekeleza mashambulio mengi ya kigaidi tangu mwaka 2016. Mnamo mwezi Novemba, mwaka 2018, ISIS-WA ilidai kuhusika na mashambulio matano nchini Chadi na Nijeria ambayo yalisababisha vifo 118. Mnamo mwezi Mei, mwaka 2019, ISIS-WA ilidai kuhusika na mashambulio mawili magharibi mwa Nijeri, ambayo yaliwaua wanajeshi 29. Mnamo mwezi Julai, mwaka 2019, wapiganaji wa ISIS-WA waliwaua wanajeshi 20 wa Nijeria na watano wa Chadi wakati wa shambulio dhidi ya kambi ya kijeshi karibu na Baga, Nijeria.
Mnamo tarehe 28 mwezi Februari, mwaka 2018, Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Marekani ilitaja ISIS-WA kuwa Kundi la Kigaidi la Kigeni chini ya kifungu 219 cha Sheria ya Uhamiaji na Uraia, kama ilivyorekebishwa. Hapo awali, mnamo tarehe 27 mwezi Februari, mwaka 2018, Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje iliitaja ISIS-WA kuwa Gaidi wa Kimataifa Mwenye Sifa Maalumu kuambatana na Amri ya Rais 13224, kama ilivyorekebishwa. Matokeo yake ni kwamba, mali yote na maslahi ya ISIS-WA katika mali, vyote vilivyoko chini ya mamlaka ya Marekani vimezuiwa, na watu wa Marekani kwa jumla wamekatazwa kushiriki kwenye miamala yoyote na ISIS-WA. Ni kosa la jinai kutoa kwa makusudi, au kujaribu au kula njama ya kutoa, msaada wa nyenzo au rasilimali kwa ISIS-WA.
