Kuhusu
Harakat al-Muqawama al-Islamiya (Hamas) ilianzishwa mnamo mwaka 1987 mwanzoni mwa machafuko ya kwanza ya Kipalestina, au Intifada ya Kwanza, kama chipukizi la tawi la Kipalestina la kundi la Muslim Brotherhood. Hamas ina mrengo wa wapiganaji unaojulikana kama Izz al-Din al-Qassam Brigades ambao umetekeleza mashambulio mengi dhidi ya Israeli na maeneo ya Kipalestina tangu miaka ya elfu moja mia tisa na tisini. Mashambulio haya yamekuwa ni pamoja na milipuko mikubwa ya mabomu dhidi ya shabaha za kiraia za Israeli, mashambulio kwa silaha ndogo, vilipuzi vya kubuniwa vya kando ya barabara, na makombora ya roketi. Hamas ilidai kuhusika na shambulio la bomu la mwezi Agosti, mwaka 2001 dhidi ya mkahawa wa pizza wa Sbarro, mjini Jerusalem, ambalo liliwaua watu 15, wakiwamo Wamarekani wawili, na kuwajeruhi wengine zaidi ya 120. Mnamo mwezi Aprili, mwaka 2016, mwanachana wa Hamas alitekeleza shambulio la kujitoa mhanga kwenye basi mjini Jerusalem ambalo liliwaua watu 20.
Mnamo tarehe 8 mwezi Oktoba, mwaka 1997, Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Marekani ilitaja Hamas kuwa Kundi la Kigaidi la Kigeni chini ya kifungu 219 cha Sheria ya Uhamiaji na Uraia, kama ilivyorekebishwa. Baadaye, mnamo tarehe 31 mwezi Oktoba, mwaka 2001, Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Marekani iliitaja Hamas kuwa Gaidi wa Kimataifa Mwenye Sifa Maalumu kuambatana na Amri ya Rais 13224, kama ilivyorekebishwa. Matokeo yake ni kwamba, mali yote na maslahi ya Hamas katika mali, vyote vilivyoko chini ya mamlaka ya Marekani vimezuiwa, na watu wa Marekani kwa jumla wamekatazwa kushiriki kwenye miamala yoyote na Hamas. Ni kosa la jinai kutoa kwa makusudi, au kujaribu au kula njama ya kutoa, msaada wa nyenzo au rasilimali kwa Hamas.
