Kuhusu
Ansar al-Dine (AAD) ilibuniwa mwishoni mwa mwaka 2011. Kufuatia mapinduzi ya mwezi Machi, mwaka 2012 yaliyoiondoa mamlakani serikali ya Mali, AAD ilikuwa miongoni mwa mashirika yaliyotwaa kaskazini ya Mali, yakaharibu sehemu za Turathi za Dunia za UNESCO, na kutekeleza fasiri kali ya sharia kwenye maeneo chini ya udhibiti wake. Mnamo mwaka 2017, AAD ilijiunga na Jama’at Nasr al-Islam wal Muslimin (JNIM), muungano mpya wa makundi yaliyoegemea upande wa al-Qa’ida ulioongozwa na kiongozi wa AAD, Iyad ag-Ghali.
Mnamo tarehe 22 mwezi Machi, mwaka 2013, Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Marekani ilitaja AAD kuwa Kundi la Kigaidi la Kigeni chini ya kifungu 219 cha Sheria ya Uhamiaji na Uraia, kama ilivyorekebishwa. Hapo awali, mnamo tarehe 21 mwezi Machi, mwaka 2013, Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Marekani ilitaja AAD kama Gaidi wa kimataifa Mwenye Sifa Maalumu kuambatana na Amri ya Rais 13224, kama ilivyorekebishwa. Matokeo yake ni kwamba, mali yote na maslahi ya AAD katika mali, vyote vilivyoko chini ya mamlaka ya Marekani vimezuiwa, na watu wa Marekani kwa jumla wamekatazwa kushiriki kwenye miamala yoyote na AAD. Ni kosa la jinai kutoa kwa makusudi, au kujaribu au kula njama ya kutoa, msaada wa nyenzo au rasilimali kwa AAD.
