Kuhusu
Tuzo kwa Mahakama inaahidi kutoa tuzo ya hadi dola milioni kumi kwa taarifa itakayosababisha kuvurugwa kwa taratibu za kifedha za Hizballah. Adham Husyan Tabaja, anayejulikana pia kama Adham Tabaja, ni mwanachama wa Hizballah ambaye hudumisha mahusiano ya moja kwa moja na wakubwa wa vipengele vya shirika vya Hizballah, kikiwamo kipengee cha Islamic Jihad, kinachoendesha shughuli za kundi hilo.
Tabaja pia anamiliki mali nchini Lebanoni kwa niaba ya Hizballah. Ndiye mmiliki mkubwa wa kampuni ya ukuzaji wa mali isiyohamishika na ujenzi ya Al-Inmaa Group for Tourism Works, ambayo iliwekewa vikwazo na Wizara ya Fedha ya Marekani mnamo mwezi Juni, mwaka 2015. Kampuni ya Tabaja ya uhandisi na ukandarasi, Al-Inmaa Engineering and Contracting, imekuwa mojawapo ya biashara kubwa na zenye ufanisi zaidi za mali isiyohamishika nchini Lebanoni tangu mwishoni mwa miaka ya tisini na imetumiwa na Hizballah kama njia ya uwekezaji. Mnamo mwaka 2006, Tabaja alitumia uhusiano wake na uongozi wa Hizballah kuijengea ukiritimba wa ujenzi kampuni ya Al-Inmaa Engineering and Contracting kwenye sehemu ya Dahieh ya mji wa Beirut inayodhibitiwa na Hizballah na kusini mwa Lebanoni. Hivi majuzi, Tabaja ametumia matawi ya Al-Inmaa Engineering and Contracting nchini Iraki kupata miradi ya mafuta na ujenzi nchini Iraki ambayo inatoa msaada wa kifedha na miundombinu ya shirika kwa Hizballah. Tabaja na kampuni zake pia wamejaribu kupata mikataba ya kibiashara yenye pesa nyingi kwenye maeneo ya Green Zone ya Baghdad, nchini Iraki. Tabaja amefanya kazi na maafisa wa Hizballah, akiwamo afisa wa masuala ya kisiasa wa Hizballah, Muhammad Kawtharani, kwa ajili ya miradi hiyo.
Mnamo tarehe 10 mwezi Juni, mwaka 2015, Wizara ya Fedha ya Marekani ilimtaja Tabaja kuwa Gaidi wa Kimataifa Mwenye Sifa Maalumu kuambatana na Amri ya Rais 13224, kama ilivyorekebishwa. Matokeo ya kutajwa huku, miongoni mwa matokeo mengine, ni kwamba mali yote na maslahi ya Tabaja katika mali, vyote vilivyoko chini ya mamlaka ya Marekani vimezuiwa, na watu wa Marekani kwa jumla wamekatazwa kushiriki kwenye miamala yoyote na Tabaja. Aidha, ni kosa la jinai kutoa kwa makusudi, au kujaribu kula njama ya kutoa, msaada wa nyenzo au rasilimali kwa Hizballah, kundi lililotajwa na Marekani kama Shirika la Kigaidi la Kigeni. Saudia pia imemtaja Tabaja na kampuni zake kama taasisi za kigaidi.
